LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

May 15, 2012

TAMKO LA NEC JUU YA KUPANDA KWA GHARAMA ZA MAISHA NCHINI.

 Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imejadili kwa kina suala la kupanda kwa gharama za maisha nchini. NEC inakiri kwamba ni kweli lipo tatizo la kupanda kwa gharama za maisha nchini.

Tatizo hili pia limezikumba karibu nchi nyingi za Afrika Mashariki na kwakweli karibu sasa lipo dunia nzima.

Baadhi ya sababu za kupanda kwa gharama za maisha hapa nchini ni pamoja na;

1. Hali mbaya ya mavuno inayotokana na uhaba wa mvua au mvua kunyesha kipindi cha nje ya msimu katika maeneo mengi nchini.
2. Kuongezeka kwa bei ya mafuta duniani, hivyo kuongezeka kwa gharama za uzalishaji wa bidhaa na usafirishaji wa mazao.
3. Kuyumba kwa thamani ya dola ya Marekani.
4. Kuwepo kwa soko huria ambapo sasa  mazao ya chakula yanapata soko nje ya nchi, na wakati mwingine kuuzwa nje kwa njia ya magendo na hivyo kusababisha uwepo wa ukubwa wa mahitaji  na hivyo kuongezeka kwa bei ya chakula nchini.
5. kuongezeka kwa walaji wakati  uzalishaji ukiwa mdogo.
6.  kutofanikiwa (ikiwemo kuhujumiwa na wafanyabiashara wasio waaminifu) kwa baadhi ya mikakati ya kudhibiti mfumko wa bei.

 Uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa.

1. Pamoja na Serikali kuendelea kuchukua hatua za muda mrefu na wa kati za kukabiliana na tatizo hili, CCM inaiagiza Serikali kuchukua hatua za haraka za muda mfupi ikiwemo kuangalia upya baadhi ya kodi katika vyakula pamoja na kodi ya ongezeko la thamani VAT katika sukari.

2. Utaratibu wa ruzuku ya mbegu na mbolea upanuliwe ili kunufaisha wakulima wengi.

3. Serikali iongeze kasi ya utekelezaji wa mpango wake wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula nchini, hasa kwa kupitia Hifadhi ya Nafaka ya Taifa, ikiwa ni pamoja na kujenga maghala zaidi ya mazao ya chakula katika maeneo ya uzalishaji wa mazao, na kutenga fedha nyingi zaidi kwa ununuzi wa mazao hayo. Pamoja na hili, mipango ifanywe kuongeza uwezo wa wakulima kuhifadhi chakula chao wenyewe na kupunguza upotevu baada ya mavuno (post-harvest losses).

3. Serikali iendelee kupanua utaratibu wake wa kutumia Hifadhi ya Nafaka ya Taifa (SGR) kama nyenzo ya kudhibiti kupanda kwa bei za vyakula.  Wakati wa uhaba wa vyakula katika maeneo ya mijini, kasi ya kupeleka chakula maeneo hayo iongezwe na utaratibu mzuri zaidi wa usambazaji wa chakula utumike ili walaji, na sio wasafirishaji na wasindikaji, wanufaike.

4. Serikali iongeze kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kilimo nchini, hasa ASDP na SAGCOT, ambayo itasaidia kumaliza tatizo la chakula nchini na kuongeza ajira na kipato kwa Watanzania walio wengi.

5. Serikali idhibiti malipo ya huduma ya ndani kwa kutumia fedha za kigeni, hasa dola za kimarekani.  Aidha, Serikali iongeze udhibiti wa Maduka na mahoteli yanayofanya biashara ya fedha za kigeni ili kuondoa hujuma kwa uchumi wa nchi inayofanywa kutokana na uhuru uliokithiri katika biashara hii.

6. Waajiri wahimizwe kupandisha mishahara na malipo mengineyo kwa wafanyakazi wao ili waweze kumudu gharama za maisha.

7. Serikali iweke jitihada zaidi za kudhibiti ulanguzi wa bidhaa muhimu na upandishaji holela wa bei za vyakula, kodi za nyumba na usafiri.


Nape Moses Nnauye
Chama Cha Mapinduzi
Ideology and Publicity Secretary

4 comments:

  1. hili ni wazo zuri katika kulinda uchumi wetu,kwani hakuna nchi yoyote duniani inaachia uchumi wake kiholela tu,hata hizo nchi zinazojiita kwamba zinafuata uchumi wa soko hazifanyi hivyo hata kidogo,kwa hiyo hili wazo limekuja wakati muafaka kabisa,ila kinachotakiwa wizara husika ya fedha iwe na nia ya dhati kabisa kufanya hivyo na isimuogope mtu yoyote baada ya sheria husika kupewa baraka na mamlaka husika,hongera halmashauri kuu ya chama kwa uamuzi huu.

    ReplyDelete
  2. Mkakati mzuri kabisa pia Nashauri kuhusu Kudhibiti Bei za Vyakula,Maana eneo hili ni Sensitive kwa Maisha ya Wananchi Serikali iandae Utaratibu ambapo ITAUZA MOJA KWA MOJA KWA WANANCHI KWA BEI NAFUU VYAKULA hv badala ya kuwauzia Wafanyabiashara Ambao baadae Huuza Kwa Bei ya Juu na Lawama kurudia Serikali

    ReplyDelete
  3. Ni jambo jema kwa ccm kuendelea kujitathminin na kubaini wapi inaweza kuboresha shughuli zake hasa kwa kuangalia dhima kubwa ya CCM kwamba ndio chama na kimbilio la wanyonge wa Tanzania, Afrika na dunia kwa ujumla wake.

    ReplyDelete
  4. HAWA WAKUU WA WILAYA WAWE CHACHU HASA YA KUTEKELEZA MAADHIMIO YENYE KUWANUFAISHA WATANZANIA, KWELI SASA NI WAKATI MCHANGO WA CHAMA KATIKA JAMII UWE WA KUZUNGUMZIKA NA UNAANZA NA SISI WENYEWE

    ReplyDelete

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages